TAASISI YA RAFIKI WA YATIMA YAWAGAWIA VIFAA VYA SHULE

DAR ES SALAAM

Taasisi ya Rafiki wa Yatima imewagawia vifaa mbalimbali vya shule kwa wanafunzi 45 ambao ni yatima wanaoishi katika mazingira ya nyumbani.

Vifaa hivyo vilivyogawiwa leo, tarehe 06 Desemba 2025 vinajumuisha begi, daftari, kalamu, na sare za shule, kwa lengo la kuwapunguzia walezi wao mzigo wa kiuchumi na kuwasaidia kuendelea na masomo yao.

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Katibu Mtendaji wa Taasisi hiyo, Mwalimu Mbwana Muda Mbwana, alisema tukio hili ni la kwanza kati ya matukio matatu yanayopangwa kufanyika kila mwaka, na kwamba huu ni mwaka wa tatu mfululizo wa kuendesha programu hii.

“Tunafanya hili tukio kila mwaka, na lengo ni kuhakikisha kuwa misaada yetu inawafikia watoto hao mara kwa mara,” alisema Mwalimu Mbwana.

Mwalimu Mbwana alibainisha sababu za chaguo la kuwalenga watoto yatima wanaoishi majumbani.

“Macho yetu mengi huwa yanalenga wale watoto walioko katika vituo. Sisi kama Rafiki wa Yatima tumebeba wajibu wa kuwatafuta na kuwatazama wale ambao wanaishi majumbani, ili nawao wafikiwe na huduma,” alisema.

Alieleza kuwa watoto hao wanaweza kuwa wamekosa baba au wazazi wote, lakini wanaishi na ndugu, mama, bibi au walezi wengine, hali inayowafanya mara nyingi kupuuzwa na misaada mbalimbali.

Akizungumzia changamoto, Mwalimu Mbwana aligusia suala la hitaji kubwa likiwa na mwitikio mdogo kutoka kwa wadau.

“Tunahitaji kukusanya vifaa kama vile viatu na sare kwa ajili ya watoto, lakini mwitikio wa wadau unakuwa mdogo. Hii inaleta changamoto katika kukidhi mahitaji yote,” alisema.

Aidha, alieleza changamoto ya imani potofu katika jamii kwamba harakati za kusaidia mayatima ni “miradi ya watu”, jambo ambalo amesema si kweli kwani taasisi yake inafanya kazi kwa uadilifu na uwazi.

“Sasa wewe unayefanya jambo kama ibada, unalifanya kwa ajili ya Mungu na malipo yake unayatarajia kwa Mungu pekee,” aliongeza Mwalimu Mbwana.

Akiongelea umuhimu wa msaada huo, alitoa mfano wa mzazi anaye lea watoto watano na mzigo wa gharama za shule.

“Kuchangia begi, daftari, sare na viatu humwondolea msongo wa mawazo huyu mlezi na kumwezesha kukabiliana na mahitaji mengine ya familia. Mchango huu ni mkubwa sana,” alieleza.

Mwalimu Mbwana alimalizia kwa kutoa wito wa dhati kwa jamii na wadau mbalimbali.

“Rai ya kwanza ni jamii tushirikiane, tusiwatenge hawa watoto… Hivyo natoa wito kwa jamii tuungane kwa pamoja katika kuwasaidia hawa watoto kijamii, kiuchumi na hata katika masuala ya kitaaluma,” alisema.

Aliomba serikali pia kuzingatia uwezekano wa kutoa ruzuku kwa taasisi zinazofanya kazi kwa uadilifu kama ya Rafiki wa Yatima, ili ziweze kupanua huduma zao.

Taasisi ya Rafiki wa Yatima, inaendelea na  mpango wake ya kuhakikisha yatima wanaoishi majumbani wanapata nafasi sawa ya kuelimika na kutimiza ndoto zao, huku ikiwa na mpango wa kuendelea na misaada kama hiyo katika miaka ijayo.





Post a Comment

Previous Post Next Post