Serikali imezindua rasmi Miongozo ya Uzalishaji Endelevu wa Ufuta na Mikunde, hatua inayolenga kuongeza tija kwa wakulima na kuhamasisha kilimo cha kisasa na endelevu.
Akizungumza katika kongamano lililowakutanisha wadau wa kilimo na uongezaji thamani kwenye mnyororo wa uzalishaji, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema miongozo hiyo itawasaidia wakulima kufanya kilimo chenye tija, kinacholinda mazingira na kuongeza kipato.Waziri Chongolo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa msukumo wa upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo za ruzuku, sambamba na upanuzi wa sekta ya kilimo nchini.
Katika hatua nyingine, amesema Wizara ya Kilimo inapanga kuanzisha Wakala wa Huduma za Ugani utakaokuwa taasisi inayojitegemea, kwa lengo la kuboresha huduma za ushauri wa kitaalamu kwa wakulima na kupunguza urasimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack, amesema tani saba za mbegu bora za ufuta tayari zimegawiwa kwa wakulima mkoani humo, hatua inayotarajiwa kuongeza mavuno na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia kilimo.
.jpg)