Na Mwandishi wetu
TAASISI ya Green Mining Awareness imewaita wadau wa sekta
ya madini nchini kujadili changamoto zinazowakabili na kupata elimu ya
uchimbaji unaozingatia kulinda mazingira.
John Paul, Meneja wa Matukio wa taasisi hiyo, amebainisha
hayo leo Aprili 2, 2026 jijini Dar es
Salaam na kufafanua kwamba wadau hao watakutana Aprili 17 mwaka huu,
Chunya mkoani Mbeya.
"Siku hiyo tutawaeleza umuhimu wa kutumia teknolojia
salama, kwa kufuata sheria, kuwa na leseni pamoja na kuepuka kutumia mbinu
zisizo salama ikiwemo za kishirikina katika uchimbaji madini," amesema.
Aidha ameongeza kwamba wanaishukuru Serikali ya awamu
sita pamoja na Wizara ya Madini chini ya Waziri Mavunde kwa kuweka
mazingira wezeshi katika sekta hiyo.
Ameongeza kuwa taasisi za kibenki ikiwemo NMB, kampuni
zinazouza na kukopesha vifaa vya uchimbaji madini, RM Kyando, Kaeser Compressor
na nyinginezo zitakuwepo ili wachimbaji waweze njia sahihi za kuweza kununua au
kukopeshwa ili wafikie ndoto zao katika uchimbaji.
Naye Anna Nyange ambaye ni Balozi wa taasisi hiyo,
amedadavua kuwa huo ni mwanzo wa
harakati za mabadiliko makubwa katika kujenga sekta ya madini iliyoendelevu na
yenye manufaa kwa wote.
"Naamini wadau wengi watajitokeza katika mkutano huo
wenye fursa zote za elimu, teknolojia na mitandao ya kibiashara ambapo
wachimbaji watakutanishwa na wafanyabishara mbalimbali ili kupata njia sahihi
ya kufanikiwa kwenye shughuli zao," amesema.
.jpeg)
